Ilifanyiwa marekebisho mara ya mwisho tarehe 09/01/2025
UTANGULIZI
Taarifa hii ya Faragha (“Taarifa”) inasimamia namna I&M Bank (T) Limited (itakayofahamika hapa kama “I&M Bank”) inavyokusanya, kutumia na kufichua/kutoa taarifa binafsi za wateja wa huduma za I&M Bank, tovuti na programu zake za mtandaoni zinazorejelea Taarifa hii (kwa pamoja zikijulikana kama “Huduma”).
Taarifa hii ya Faragha inahisisha bidhaa na huduma zote ambazo watejawetu wana zipata kutoka kwetu, ikiwamo akaunti, mikopo, kadi, uwekezaji na bima, ambazo zote ni sehemu ya Huduma.
Kwa muktadha huu, “taarifa binafsi” zina maana ya taarifa zinazomhusu mtu binafsi anayetambulika au anayeweza kutambulika.
Popote maneno “Wewe” au “Wako” yanapotumika, yana maana ya mteja, mtu yeyote aliyeidhinishwa kwenye akaunti yako/zako, na mtu yeyote anayeshughulika nasi kwa niaba yako, ikiwamo mwakilishi chini ya Hati ya Uwakilishi (Power of Attorney), wasimamizi wa mirathi, wawakilishi binafsi, wanufaika na wadhamini.
Popote maneno “Sisi” au “Kwetu” yanapotumika, yana maana ya I&M Bank (T) Limited, ambaye ndiye mdhibiti mkuu wa taarifa zako binafsi kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Tanzania ya mwaka 2022.
Tunakushauri kusoma Taarifa hii yote kwa makini.
TAARIFA BINAFSI TUNAZOKUSANYA KUPITIA HUDUMA
I&M Bank (T) Limited hukusanya na kutumia baadhi ya taarifa binafsi ili kuweza kuendesha na kukuwezesha kukupatia Huduma, kwa mujibu wa sheria na kanuni za ulinzi wa taarifa za Tanzania, ikiwamo picha za kamera na rekodi za video.
Pale taarifa binafsi zinapotolewa ndani ya Kundi la I&M, utoaji huo wa taarifa binafsi utafanywa kwa kuzingatia Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Tanzania na ulinzi sawa utatumika. Taarifa hizi zinajumuisha zile unazotupatia wewe mwenyewe, zile tunazokusanya pale unapotembelea au kutumia Huduma, pamoja na taarifa fulani zinazopatikana kwenye vyanzo vya umma.
TAARIFA UNAZOTUPATIA
Tunakusanya taarifa binafsi unazotupatia kwa hiari unapotumia Huduma. Taarifa hizi zinajumuisha, bila ukomo: jina lako, jinsi, tarehe ya kuzaliwa na taarifa zingine binafsi; anwani zako za barua pepe, namba za simu na taarifa zingine za mawasiliano; taarifa za wasifu; taarifa za sauti na picha, taarifa za mitandao ya kijamii; mawasiliano yako na huduma kwa wateja wetu kwa njia ya simu, ana kwa ana, barua pepe au njia nyinginezo; maoni na mrejesho, ikiwamo tafiti za soko, kupitia tovuti, programu za wavuti au simu; mapendeleo ya mtandaoni kama vile vidokezo; na taarifa za kibiashara kama jina la kampuni yako na sekta unayofanya kazi.
Kupitia taarifa tunazokusanya kutoka kwako, tutahakikisha taarifa zako zinahifadhiwa kwa usahihi kama ulivyotupatia. Wewe una wajibu wa kutuarifu mara moja endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote katika taarifa zako ili tuzirekebishe na kuzihifadhi zikiwa sahihi na za wakati huo.
Endapo utatupatia taarifa za mtu mwingine zinazohitajika kwa matumizi ya Huduma, utawajibika kumjulisha mtu huyo kuhusu Taarifa hii ya Faragha na kuhakikisha anakubali matumizi ya taarifa zake kama ulivyotupatia.
Tunaweza kurekodi na kufuatilia mawasiliano yako nasi kupitia simu, mikutano ya ana kwa ana, barua, barua pepe, mazungumzo ya mtandaoni au njia nyinginezo ili kuthibitisha maelekezo yako, kuboresha Huduma zetu, kulinda usiri na usalama wa taarifa zako au kudhibiti hatari zinazoweza kujitokeza.
TAARIFA TUNAZOKUSANYA KUHUSU MATUMIZI YAKO YA HUDUMA
Tunakusanya taarifa kuhusu namna unavyotumia Huduma na kifaa unachotumia kufikia Huduma, ikiwamo kurasa unazotembelea; maudhui unayowasilisha; mwingiliano wako na watumiaji wengine; taarifa zinazopatikana wakati wa kuendesha au kusaidia Huduma; pamoja na taarifa za matumizi yako ya intaneti kama anwani ya IP, tovuti unazotokea au unakoelekea, aina ya kivinjari, mfumo wa uendeshaji na mtoa huduma wa intaneti.
Iwapo utatumia Huduma kupitia kifaa cha mkononi, tunaweza pia kukusanya taarifa kuhusu mtoa huduma wako wa simu, IMSI, IMEI na aina ya kifaa cha mkononi.
Sisi (na wachakataji wetu wa taarifa) tunatumia teknolojia mbalimbali kukusanya taarifa hizi, ikiwamo vidakuzi (cookies) na “web beacons”. Vidakuzi ni faili ndogo za data zinazohifadhiwa kwenye kifaa chako na hutusaidia kuboresha Huduma na uzoefu wako, kutambua vipengele vinavyotumika zaidi na kuhesabu idadi ya watembeleaji. “Web beacons” ni picha za kielektroni zinazotumika kwenye Huduma au barua pepe zetu ili kusaidia kusambaza vidakuzi, kuhesabu watembeleaji na kuelewa matumizi na ufanisi wa kampeni.
Tunaweza pia kutumia mifumo ya kiotomati kutusaidia katika kufanya uamuzi fulani unaohusiana na matumizi yako ya Huduma, ikiwamo uamuzi kuhusu tathmini ya mkopo, utambuzi wa udanganyifu au uhalifu wa kifedha, upangaji wa bei za bima au tathmini ya hatari za uwekezaji.
UTANGAZAJI WA MTANDAONI NA HUDUMA ZA UCHAMBUZI WA TAKWIMU ZINAZOTOLEWA NA WATU WENGINE
Tunaweza kuruhusu wahusika wengine kutoa huduma za uchambuzi wa takwimu (analytics) na kuendesha matangazo kwa niaba yetu katika tovuti mbalimbali na programu za simu, kwa lengo la kuboresha Huduma zetu. Wahusika hawa wanaweza kutumia vidakuzi (cookies), “web beacons”, vitambulishi vya vifaa (device identifiers) na teknolojia nyingine kukusanya taarifa kuhusu matumizi yako ya Huduma na tovuti au programu nyingine, ikiwamo anwani yako ya IP, aina ya kivinjari cha intaneti, taarifa za mtandao wa simu, kurasa ulizotembelea, muda uliotumia kwenye kurasa au programu, viungo ulivyobofya na taarifa za ubadilishaji (conversion information).
Taarifa hizi zinaweza kutumiwa na sisi pamoja na wachakataji wetu wa taarifa kwa madhumuni mbalimbali ikiwamo kuchambua na kufuatilia takwimu, kubaini umaarufu wa maudhui fulani, kuwasilisha matangazo na maudhui yanayolengwa kulingana na maslahi yako kupitia Huduma zetu na tovuti nyingine, pamoja na kuelewa kwa undani zaidi shughuli zako za mtandaoni.
MATUMIZI YA TAARIFA BINAFSI
Tunatumia taarifa binafsi tunazokusanya ili kutoa, kuendesha, kudumisha na kuboresha Huduma zetu, au pale tunapokuwa na sababu nyingine za kisheria za kuzitumia. Aidha, tunazitumia kwa madhumuni yafuatayo:
- Kukutumia taarifa za kiufundi, masasisho ya jumla, ujumbe wa kirafiki, tahadhari za kiusalama, pamoja na ujumbe wa msaada na kiutawala (kama vile mabadiliko ya masharti, vigezo na sera zetu), na kujibu maoni, maswali na maombi yako kwa huduma kwa wateja;
- Kupokea na kujibu mawasilisho yako kupitia Huduma, ikiwamo mawasilisho kupitia tovuti ya I&M Bank, programu za wavuti na simu, mitandao ya kijamii, pamoja na mawasiliano kwa Huduma kwa Wateja;
- Kukuwezesha kushiriki katika kura za hiari na tafiti (tunaweza kutumia wahusika wengine kutoa vivutio vya ushiriki, na unaweza kuhitajika kutoa taarifa zako za mawasiliano kwa mhusika wa tatu ili kutekeleza ofa ya vivutio);
- Kuwasiliana nawe kuhusu bidhaa, huduma na matukio yanayotolewa na I&M Bank na wengine, na kukupatia habari na taarifa tunazoona zinaweza kukuvutia;
- Kufuatilia na kuchambua mienendo, matumizi na shughuli zinazohusiana na Huduma zetu;
- Kuendeleza bidhaa na huduma mpya na kuboresha bidhaa na huduma zilizopo;
- Kugundua, kuchunguza na kuzuia miamala ya udanganyifu na shughuli nyingine zisizo halali, pamoja na kulinda haki na mali za I&M Bank na wengine (kwa maslahi ya umma);
- Kutekeleza, kulinda na kutetea haki zetu za kisheria;
- Kutuwezesha kuingia au kutekeleza makubaliano tuliyo nayo;
- Kutii sheria, kanuni au wajibu wowote wa kisheria; na
- Kutekeleza madhumuni mengine yoyote uliyoelezwa wakati wa ukusanyaji wa taarifa.
JINSI TAARIFA BINAFSI ZINAVYOTOLEWA
Tunaweza kuwapatia watu wengine taarifa zako binafsi pale inapokuwa halali kufanya hivyo, kama ilivyoelezwa katika Taarifa hii, ikiwamo:
- Kwa wachakataji wetu wa taarifa wanaohifadhi, kusimamia, kudumisha au kutoa huduma nyingine zinazohusiana na Huduma;
- Kushirikiana na mamlaka za umma na serikali, mahakama na vyombo vya utekelezaji wa sheria, ili kujibu maombi au kutoa taarifa kwa mujibu wa sheria zilizopo;
- Kwa sababu nyingine za kisheria, ikiwamo kufuatilia utekelezaji wa masharti na vigezo vyetu, kulinda haki, faragha, usalama au mali zetu, washirika wetu, wewe au wengine, kuzuia uhalifu na kwa madhumuni ya usimamizi wa hatari;
- Kuhusiana na mauzo au miamala ya kibiashara, kama vile kwa mnunuzi au washauri wake endapo kutatokea upangaji upya wa biashara, muunganiko, mauzo, ubia, uhawilishaji au uhamishaji wa biashara, mali au hisa zetu zote au sehemu yake (ikijumuisha taratibu za kufilisika au zinazofanana);
- Kwa madhumuni ya kutangaza Huduma kwako au kwa wengine pale ulipotoa idhini yako;
- Kuwezesha maslahi yetu halali ikiwamo, bila ukomo, utoaji wa mikopo, urejeshaji wa madeni, usimamizi wa mali au fedha, pamoja na uendeshaji wa akaunti.
Tunaweza pia kushirikisha taarifa zilizokusanywa kwa ujumla, zilizofichwa utambulisho (pseudonymised) au zisizotambulika (anonymised), ambazo haziwezi kutumika kukutambua, kwa lengo la kulinda haki zako za faragha.
WATOTO
Huduma zote tunazotoa kwa watoto zinaendana na matakwa ya kisheria ya ulinzi wa taarifa. Hii inajumuisha idhini inayotolewa na mzazi au mlezi wa mtoto pamoja na uthibitisho wa umri. Endapo una sababu ya kuamini kuwa mtoto ametoa taarifa binafsi kwetu, tafadhali wasiliana nasi na tutachukua hatua za kufuta taarifa hizo kutoka kwenye kanzidata zetu.
VIUNGO VYA TOVUTI ZINGINE
Huduma zinaweza kuwa na viungo vinavyoelekeza kwenye tovuti zingine. Tafadhali tambua kuwa I&M Bank (T) Limited haiwajibiki kwenye sera au taratibu za faragha na usalama wa taarifa za tovuti zingine. Unashauriwa kusoma kwa makini sera na taarifa za faragha na usalama wa taarifa za tovuti zingine unazotembelea kupitia Huduma. Taarifa hii inatumika tu kwa taarifa binafsi zinazokusanywa kupitia Huduma zetu.
USALAMA
Tunatumia hatua stahiki za kiufundi na kiutawala kulinda taarifa binafsi ndani ya taasisi yetu dhidi ya upotevu, wizi, uvunjaji wa usalama na matumizi, ufichuzi au mabadiliko yasiyoidhinishwa. Tumechukua hatua mbalimbali kulinda taarifa zako ikiwamo usimbaji wa taarifa (encryption) na mbinu nyingine za kiusalama.
Pia tunawataka wafanyakazi wetu na wahusika wengine tunaowashirikisha kufuata sera zetu za ndani na kutekeleza hatua zote za uzingatiaji wa sheria kwa mujibu wa sheria na kanuni husika, kwa kusaini makubaliano ya usiri, makubaliano ya uchakataji wa taarifa na nyaraka nyingine za kisheria ili kulinda taarifa zako.
Tafadhali rejea maudhui yafuatayo ili kufahamu wajibu wako katika kudhibiti faragha na taarifa zako binafsi.
DHIBITI FARAGHA NA TAARIFA ZAKO
MAWASILIANO YA MASOKO
Tunaweza kutumia taarifa zako kukupatia maelezo kuhusu Huduma zetu pamoja na huduma nyingine tunazozitangaza. Tunaweza kukutumia maombi ya kukubali (opt-in) kupokea mawasiliano ya masoko kwa njia ya barua, barua pepe, simu, ujumbe mfupi (SMS), mitandao ya kijamii au kupitia huduma zetu za mtandaoni.
Unaweza kubadilisha namna unavyopenda kupokea mawasiliano ya masoko, au kuacha kabisa kupokea mawasiliano hayo wakati wowote. Endapo hutaki tena kupokea mawasiliano ya masoko kutoka I&M Bank, unaweza kujiondoa (opt-out/unsubscribe) kwa kufuata maelekezo yaliyomo kwenye kila ujumbe wa masoko unaotumwa kwako au kwa kuwasiliana na Kituo cha Huduma kwa Wateja cha I&M Bank. Tutajitahidi kutekeleza ombi lako haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa hali halisi.
Tafadhali zingatia kuwa hata ukijiondoa kwenye mawasiliano ya masoko, bado tunaweza kukutumia ujumbe wa kiutawala ambao huwezi kujiondoa, ikiwemo taarifa kuhusu mabadiliko ya masharti na vigezo, masasisho ya mifumo au mawasiliano yanayohitajika kwa uzingatiaji wa matakwa ya kisheria.
VIDAKUZI
Vivinjari vingi vya tovuti vimewekwa kukubali vidakuzi kiotomati. Iwapo unapendelea, unaweza kubadilisha mipangilio ya kivinjari chako ili kuondoa au kukataa vidakuzi. Tafadhali fahamu kuwa kuchagua kuondoa au kukataa vidakuzi kunaweza kuathiri upatikanaji na utendaji wa Huduma zetu.
MABADILIKO YA TAARIFA HII
Mara kwa mara, tunaweza kufanya marekebisho ya Taarifa hii. Mabadiliko yanaweza kufanyika kwa sababu mbalimbali ikiwamo, bila ukomo, kuakisi mabadiliko ya sekta, marekebisho ya sheria au mabadiliko ya wigo wa Huduma zetu. Unaweza kujua lini Taarifa ilisasishwa mara ya mwisho kwa kuangalia tarehe iliyo mwanzoni mwa Taarifa hii. Mabadiliko yoyote yataanza kutumika mara tu Taarifa iliyorekebishwa itakapochapishwa kwenye Huduma zetu.
WASILIANA NASI
Iwapo una maswali yoyote kuhusu Taarifa hii, tafadhali wasiliana nasi kupitia njia zetu rasmi zilizopo au kupitia Msimbo wa QR (QR Code) uliotengenezwa na benki.
MSINGI WA KISHERIA WA UCHAKATAJI WA TAARIFA
Tunapochakata taarifa zako binafsi, tutafanya hivyo tu katika hali zifuatazo:
- Pale inapohitajika kutumia taarifa zako binafsi kutekeleza wajibu wetu chini ya masharti na vigezo vyetu (mfano, kuwezesha ushiriki wako katika kura na tafiti za hiari);
- Pale tunapokuwa na maslahi halali ya kuchakata taarifa zako binafsi, ikiwemo kukutumia mawasiliano ya masoko, kukuarifu mabadiliko ya Huduma, pamoja na kutoa, kulinda na kuboresha Huduma zetu;
- Pale inapohitajika kuchakata taarifa zako ili kutii wajibu wa kisheria; na
- Pale tunapokuwa na idhini yako. Endapo idhini ndiyo msingi wa kisheria wa uchakataji, una haki ya kuiondoa wakati wowote kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.
HAKI ZAKO
Tunataka kuhakikisha unatambua haki zako kuhusiana na taarifa zako binafsi tunazochakata. Haki zako na mazingira ya matumizi yake zimefafanuliwa katika jedwali lifuatalo.
Iwapo ungependa kutumia haki zako, una maswali kuhusu matumizi ya taarifa zako binafsi ambayo hayajajibiwa hapa, au ungependa kuwasilisha malalamiko kuhusu haki zako, tafadhali wasiliana nasi kama ilivyoelezwa hapa chini.
HAKI ZAKO KUHUSU TAARIFA BINAFSI
| Haki |
Maelezo |
| Kufahamishwa |
Una haki ya kufahamishwa namna tunavyotumia taarifa zako binafsi. |
| Upatikanaji |
Una haki ya kupata taarifa binafsi tunazozihifadhi zinazokuhusu. |
| Kupinga |
Una haki ya kupinga uchakataji wa taarifa zako binafsi kwa sehemu au kwa ujumla. |
| Marekebisho ya taarifa |
Una haki ya kusahihisha taarifa zisizo sahihi au zinazopotosha na kukamilisha taarifa zisizokamilika. |
| Ufutaji wa taarifa potofu |
Una haki ya kuomba kufutwa kwa taarifa potofu au zinazopotosha tunazozihifadhi. |
| Uhamishaji wa taarifa |
Una haki ya kuomba nakala ya taarifa zako binafsi iwasilishwe kwa taasisi nyingine. |
| Kufutwa (Erasure) |
Una haki ya kuomba taarifa zako binafsi zifutwe. |
| Masoko |
Una haki ya kupinga masoko ya moja kwa moja. |
| Kuondoa idhini |
Una haki ya kuondoa idhini yako wakati wowote. |
MAWASILIANO YA OFISA ULINZI WA TAARIFA
Ofisa Ulinzi wa Taarifa,
I&M Bank (T) Limited,
I&M House @1046, Barabara ya Haile Selassie
S.L.P 1509,
Dar es Salaam, Tanzania
Mawasiliano mbadala:
Barua pepe: Gabriel.Mlinga@imbank.co.tz
Au: Tembelea tawi lolote la karibu la I&M Bank.
UHIFADHI WA TAARIFA
Tunatunza taarifa zako binafsi kwa muda unaohitajika kwa mujibu wa sheria na kanuni husika. Kwa mfano, tutahifadhi taarifa zako za kibenki kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwisho wa uhusiano wetu nawe, kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na ya udhibiti. Aidha, tunaweza kuzitumia kwa madhumuni yetu halali kama vile kusimamia akaunti yako, kushughulikia migogoro ya kisheria, udanganyifu au uhalifu wa kifedha, pamoja na kushughulikia mahitaji ya mamlaka za udhibiti au masuala mengine ya kisheria yanayoweza kujitokeza.
Pale ambapo hatuhitaji tena kutunza taarifa zako kwa kipindi hicho, tunaweza kuziharibu, kuzifuta au kuzibadilisha ziwe zisizotambulika (anonymise) mapema, ama kwa ombi lako au kwa uamuzi wetu.
UHAMISHAJI WA TAARIFA
Taarifa zako binafsi zinaweza kuhifadhiwa na kuchakatwa katika nchi yoyote ambako tuna ofisi au miundombinu, au ambako tunashirikisha wadhibiti au wachakataji wa taarifa. Pale taarifa zinaposhirikishwa, tutahakikisha zinapewa kiwango stahiki cha ulinzi na kwamba uhamishaji huo ni halali, kwa kuzingatia sheria na kanuni husika za ulinzi wa taarifa.
UPATIKANAJI
Iwapo unahitaji taarifa hizi katika muundo mwingine, tafadhali wasiliana nasi kupitia njia zetu zote rasmi zinazopatikana au kupitia kiungo kilichotolewa.
KURIDHIA
Matumizi yako ya Huduma yanaashiria kuwa unaridhia matumizi ya taarifa zako binafsi na I&M Bank kwa madhumuni mahsusi yaliyoainishwa katika Taarifa hii ya Faragha. Taarifa hii ya Faragha imewasilishwa kwako kupitia tovuti yetu, na umefanya uamuzi wa kufahamu na kuruhusu I&M Bank kuchakata taarifa zako binafsi kama ilivyoelezwa humu.
MAWASILIANO YA OFISA ULINZI WA TAARIFA
Simu: +255 784 107 999
Barua pepe: Gabriel.Mlinga@imbank.co.tz
I&M Bank (T) Limited,
1046 I&M House, Barabara ya Haile Selassie,
S.L.P 1509,
Dar es Salaam,
Tanzania.